Kiungo wa Bayern Munich Xabi Alonso ametangaza kustaafu soka wakati mkataba wake utakapomalizika kipindi cha kiangazi, msimu huu.
Alonso mwenye umri wa miaka 35, alishinda vikombe na vilabu vya Liverpool, Real Madrid na Bayern, na Kombe la Dunia, akiwa na timu ya taifa ya Hispania mwaka 2010.
Alonso aliiambia Televisheni ya Bayern: "Haikuwa maamuzi mepesi kufanya, lakini ni wakati muafaka".
Alonso alijiunga na Liverpool kutoka klabu ya Real Sociedad mwaka 2004 na alikuwa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichotwaa Champions League mjini Istanbul, ukiwa ni msimu wake wa kwanza, Wekundu wa Anfield, walitoka nyuma kwa mabao 3-0, hadi mapumziko, na kuitoa AC Milan, kwa penati.
Aliondoka Liverpool na kujiunga na Real Madrid mwaka 2009 na kutwaa kikombe cha Champions League kwa mara nyingine, na pia kutwaa ubingwa wa Hispania, kabla ya kutimukia Ujerumani mwaka 2014, na kuisaidia Bayern Munich kutwaa vikombe viwili vya Bundesliga.