Serikali ya Tanzania imesema kuwa raia wake wanane wanaoshikiliwa na mamlaka nchini Malawi sio wapelelezi, bali ni wanaharakati wanaopinga uchimbaji wa madini ya uranium.
Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Augustine Mahiga amekana ripoti zilizotolewa na vyombo vya habari vya Malawi kuwa Watanzania hao ni wapelelezi.
Amesema serikali imethibitisha kuwa watanzania hao wanafanya kazi kwenye kampuni isiyo ya serikali ya Ujerumani, ambayo inatetea kusimamishwa kwa uchimbaji na matumizi ya uranium.
Ameongeza kuwa Watanzania hao walikwenda Malawi kutafuta ufahamu zaidi kuhusu uchimbaji wa uranium na madhara yake.