Shirika la Afya Duniani WHO limesema kwa sasa ukame nchini Somalia unatishia maisha ya watu milioni 1.5 na kati ya hao, ni nusu tu ndio wanaweza kupata huduma ya afya ya kimsingi. Watu wa Somalia wanaathiriwa na ukame mkali unaosababisha uhaba mkubwa wa chakula na kueneza maradhi kama vile kipindupindu na surua.
WHO imesema itatoa misaada kadiri iwezekanavyo kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kupeleka wafanyakazi, dawa na vifaa vya matibabu kwenye sehemu zenye ukame.
Hali ya kibinadamu nchini Somalia inaendelea kuzorota na kuna hatari kubwa ya kutokea baa la njaa litakalokuwa la tatu katika miaka 25 iliyopita. WHO inasema inajitahidi kukusanya dola milioni 10 kwa ajili ya kusaidia nchi hiyo.