Baada ya jana hasimu wake Diamond Platinumz kuongea sana jana kwenye kipindi cha XXL
cha Redio Clouds, Msanii Omary Nyembo Al-maarufu kama Ommy Dimpoz leo naye alipata wasaa na kuvunja ukimya kuhusu swahiba wake huyo wa siku nyingi akiweka wazi kwamba hawakuwahi kuwa na tofauti kubwa kiasi cha kugombana bali aliamua kujiweka pembeni baada ya kuona mwenzake anaanza kufanya mambo mengi bila kumshirikisha jambo ambalo lilikuwa kinyume na utaratibu wao.
Akakana mbele ya wasikilizaji kuhusiana na kauli ya swahiba wake huyo wa zamani ya kwamba anaomba watu wawapatanishe, ila akasema kwamba mmoja kati ya mameneja wa Diamond aitwae Sallam Sharaff ndio aliyekuwa akimshawishi Dimpoz kupiga simu kwa Diamond ili wamalize kitu ambacho Dimpoz amekataa na kuomba itafutwe namna nyingine na sio simu.
Katika mahojiano hayo yanayosadikiwa kusikilizwa na mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya, Dimpoz amekataa kwamba hashindani na Diamond, na wala hana wivu naye bali yeye anafanya muziki wake unaofuata ratiba alizojiwekea.
Alipoulizwa kuhusiana na Beef yao, akasema iendelee kwa minajili ya kutengeneza pesa na kukiri kwamba yuko tayari kutumbuiza jukwaa moja na Diamond wakati wowote itakapotangazwa .