Maelfu ya watu wakimbia makazi yao baada ya moto mkubwa kuendelea kuenea na kukaribia kufika katika mji wa Haifa, kaskazini mwa nchi hiyo.
Moto mkubwa ambao umekuwa ukiwaka kwa siku kadha Israel sasa unakaribia mji waHaifa kaskazini mwa nchi hiyo. Moto huo umesababisha uharibifu mkubwa. Watu karibu 50,000 katika mitaa minane wametakiwa kuhama. Wazimamoto wanaendelea na juhudi za kukabiliana na moto huo, ingawa umeathiri maeneo makubwa na wazimamoto hao ni wachache. Wanahitajika pia kuwalinda raia na nyumba zisishike moto.
Maelfu ya watu wamehama makwao Haifa, wakijaribu kunusuru mali yao.
Hakuna taarifa zozote za watu kuumia vibaya lakini watu kadha wamepelekwa hospitalini wakikabiliwa na matatizo kutokana na kupumua hewa iliyojaa moshi.
Maeneo yanayokabiliwa na moto huo yalikuwa yamekabiliwa na kiangazi kwa miezi miwili. Mawaziri wanasema huenda moto huo uliwashwa makusudi.
Misitu iliyo karibu na Jerusalem pia inaweza kushika moto, Israel imepokea usaidizi kutoka Urusi, Uturuki, Ugiriki, Italia, Croatia na Cyprus.