
Beki wa klabu ya AFC Bournemouth Tyrone Mings, amefungiwa kucheza michezo mitano ilio chini ya chama cha soka nchini England (FA), baada ya kukutwa na hatia ya kumkanyaga kwa makusudi mshambuliaji wa Man Utd Zlatan Ibrahimovic.
Mings alifanya tukio hilo wakati wa mchezo wa ligi kuu uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita kwenye uwanja wa Old Trafford, na alipowasilisha utetezi wake mbele ya FA alikana tuhuma hizo.
Katika utetezi wake, beki huyo mwenye umri wa miaka 23, alidai hakumkanyaga kwa makusudi mshambuliaji huyo kutoka nchini Sweden, bali alikua katika harakati za kuukwepa mkono wa Zlatan na kwa bahati mbaya alimkanyaga kichwani.
Maamuzi hayo ya FA yameusikitisha uongozi wa AFC Bournemouth ambao umedai ni pigo kubwa sana kwao kumkosa Mings katika michezo mitano, ambayo itakua na umuhimu mkubwa.
Mings ataanza kuitumikia adhabu yake mwishoni mwa juma hili kwa kukosa mchezo dhidi ya West Ham, kisha Swansea (Machi 18), Southampton (Aprili Mosi), Liverpool (April 5) na Chelsea (April 8).
Ming anaratajiwa kurejea uwanjani Aprili 15 ambapo AFC Bournemouth itakua na kibarua cha kuwakabili Tottenham.
Kwa upande wa Zlatan Ibrahimovic ambaye alifunguliwa mashataka ya kumpiga kiwiko Mings, kitendo ambacho kilitazamwa kama kurudisha mashambulizi, amefungiwa michezo mitatu.