Utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Itigi umeonekana kuwa wenye kasi inayoridhisha licha ya halmashauri hiyo kuanzishwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kaimu Kaibu Tawala Mkoa wa Singia Buhacha Baltazari Kichinda ametoa tathmini hiyo wakati wa kikao na wataalamu wa halmashauri hiyo ambapo wamejadili mikakati ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji.
Kichinda amesema ofisi ya Mkuu wa Mkoa haina wasiwasi kuhusu halmashauri kutekeleza na kusimamia miradi ya maji huku matarajio yakiwa ni ifikapo Juni 2018, asilimia ya upatikanaji wa maji ipande kutoka asilimia 34 za sasa hadi kufikia lengo la mkoa la asilimia 72.
“Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri mnaonyesha dhahiri mmejitosa kuwapunguzia wananchi adha ya kutafuta maji huku wakiacha kwa muda shughuli zao za uzalishaji mali, nina imani mtafikia asilimia 72 hata kabla ya Juni 2018 kwakuwa fedha mnazo na pia mnafanya usimamizi wa karibu wa miradi”, amesisitiza Kichinda.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida na hata halmashauri ya Itigi haina mito inayotiririsha maji mwaka mzima hivyo kusababisha uhaba wa upatikanaji wa maji katika kipindi cha kiangazi huku wananachi wakitegemea mabwawa na visima ambavyo vinatakiwa kujengwa na serikali.
“Kipidi cha Kiangazi kwakweli utawahurumia wananchi wanavyosumbuka kutafuta maji, wanatumia muda mwingi huko na kujikuta wana muda kidogo wa kuzalisha mali, hali hii haipendezi na nina imani pia viongozi wa Itigi hili haliwapendezi ndio maana mmeweka nia ya dhati kulitatua ili wananchi wapate muda mwingi wa kuzalisha kwaajili ya maendeleo ya Mkoa na taifa letu”, amefafanua Kichinda.
Naye Mhandisi wa Maji Mkoa wa Singida Lydia Joseph amesema endapo halmahauri hiyo itasimamia kwa umakini na haraka kukamilika kwa miradi ya Itigi mijini, Kitaraka na Aghondi itasaidia ongezeko la upatikanaji wa maji kwa asilimia 20.
Kwa upande wake Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Itigi Evaristo Mgaya amesema halmashauri hiyo inatekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Rungwa, Ipande, Sanjaranda, Itigi, Kitaraka na Aghondi huku kukiwa na mradi wa visima 16 vya ‘windmill’ katika vijiji 12.
Mgaya ameeleza kuwa miradi hiyo itakamilika ndani ya kipindi cha mwaka huu wa fedha yaani kabla ya Juni 2018 hivyo kuongeza upatikanaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 72.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi Luhende Pius Shija amesema wamewajibika sana kuboresha upatikanaji wa huduma za maji ambazo ni muhimu katika kukuza uchumi.
Luhende amesema licha ya kuendelea kutekeleza miradi iliyoko kwenye bajeti pia yeye na wataalamu wa idara ya maji wameongeza jitihada kwa kuwasilisha maombi mengine ya kuonezewa fedha za miradi ya maji ambapo tayari wamekubaliwa hali itayaongeza zaidi upatikanaji wa maji.
PICHANI JUU: 1. Kaimu Kaibu Tawala Mkoa wa Singia Buhacha Baltazari Kichinda akikagua ukarabati wa bwawa la Itagata lililoko halmashauri ya Wilaya ya Itigi, kukamilika kwa bwawa hilo kutasaidia usambazaji wa maji kwa vijiji jirani pamoja na kuwezesha skimu ya umwagiliaji katika kijiji cha Itagata.