TAARIFA KWA UMMA
Serikali imewataka Wachimbaji Wadogo wa Madini kuachia maeneo ya Namba 1, 2, 3, 4 na 6 katika eneo la Mwakitolyo lililo ndani ya Leseni ya utafutaji Madini Na. PL 5044/2008 inayomilikiwa na Kampuni ya Pangea Minerals Limited kuanzia tarehe 29/11/2016.
Wachimbaji hao pia wametakiwa kuachia eneo la Mahiga lenye Leseni za Uchimbaji Madini Na. ML 448/2011 na ML 535/2014 zinazomilikiwa na Kampuni ya Henan Afro-Asian Geo-Engineering.
Wakati huohuo, Serikali imeitaka Kampuni hiyo ya Pangea Minerals kuachia eneo la Mwakitolyo Namba 5 ili litengwe kwa ajili ya uchimbaji mdogo.
Akitoa agizo hilo la Serikali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani aliwataka wadau wa Madini katika eneo hilo la Mwakitolyo kushirikiana kumaliza mgogoro huo uliokwamisha uendelezaji wa Mgodi mkubwa katika eneo hilo kwa muda mrefu.
Sambamba na hilo, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje amewapa notisi Wachimbaji Wadogo ya kusitisha uchimbaji katika maeneo ya Leseni za kampuni ya Pangea na Henan kuanzia tarehe 29/11/2016 na kuondoka katika maeneo hayo.
Aidha, Notisi hiyo imetoa siku 14 kuanzia tarehe 29/11/2016 hadi 12/12/2016, kwa Wachenjuaji Madini kuachia maeneo hayo ya leseni za Pangea na Henan.
Wachimbaji hao Wadogo wametakiwa waombe kumilikishwa maeneo yaliyotengwa kwa uchimbaji mdogo katika eneo Namba 5, Mwakitolyo, Wilayani Shinyanga na Buzwagi, Wilayani Kahama.
Kampuni ya Pangea Minerals Limited, ilimilikishwa Leseni ya Utafutaji Madini Na. PL 5044/2008 tangu mwaka 2008 na kufikia hatua ya upembuzi yakinifu. Serikali imemtaka Mwekezaji huyo kukamilisha hatua za uanzishaji Mgodi katika eneo hilo.
Imetolewa na,
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
Novemba 30, 2016