Shirika la Umoja wa Matifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limefanya uzinduzi wa kozi ya maadili kwa walimu ambao wanafundisha vyuo vya afya na sayansi kutoka ndani na nje ya nchi. Akizungumza katika ufunguzi wa kozi hiyo, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues alisema UNESCO imeandaa kozi hiyo ili kuwajengea uwezo kuhusu maadili mema ya kazi walimu hao ili hata wanafunzi wanaowafundisha wawe na maadili mema sasa na hata baada ya kuhitimu masomo yao.
Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues akitoa neno la ufunguzi katika kozi ya siku nne kuwa walimu wa vyuo vya afya wa ndani na nje ya nchi.
"Kwenu wanufaika wa kozi hii ambao itafanyika kwa siku nne, ni matumaini yangu kozi hii ya siku nne itatumika kikamilifu katika maisha yenu ya kila siku, ikiwa kama ni mkufunzi, mwanafunzi au katika tafiti zenu za kisayansi, na utakuwa balozi wa UNESCO kwa kusambaza elimu kwa wengine, "Jambo la muhimu ni kujenga uelewa ili kuhakikisha kama nchi inapambana na changamoto kubwa za kimaadili ambazo zinaikabili kwa sasa na baadae. UNESCO itaendelea kushirikiana na Muhimbili na wadau wengine wa ajili ya kusaidia Tanzania," alisema Zulmira.
Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues akizungumza na washiriki wa kozi ya maadili kwa walimu wa vyuo vya afya.
Kwa upande wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili, Prof. Ephata Kaaya alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa walimu hao na kuwahakikishia kuwa kila mshiriki hataondoka bure kwani watapewa mafunzo na wakufunzi wenye uwezo mkubwa. "Niwahakikishie washiriki wote wa kozi hii ambao mnatoka ndani na nje ya nchi kuwa mafunzo haya yatawaongezea uelewa kuhusu maadili mema, hili tatizo sio la Tanzania pekee hata Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda wote wanakabiliwa na hili tatizo kama ilivyo kwetu," alisema Prof. Kaaya.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili, Prof. Ephata Kaaya akizungumza kuhusu kozi ya maadili kwa walimu wa vyuo vya afya na kuahidi kuwa mafunzo hayo yatakuwa bora na ambayo yatakuwa msaada mkubwa kwao.
Aidha Prof. Kaaya aliishukuru UNESCO kwa kutoa mafunzo hayo na kuwaomba kuendeleza ushirikiano uliopo kati yao.
Baadhi ya washiriki wa kozi ya maadili ya siku nne iliyoandaliwa na UNESCO.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja.