Na Mwandishi Wetu
Pete iliyotengenezwa kwa madini ya Tanzanite yenye thamani ya shilingi za kitanzania Milioni nne, huenda ikawa mali ya wapendanao watakaokuwa na bahati, maana ni miongoni mwa zawadi nono zitakazotolewa katika onesho la wapendanao lililopachikwa jina la Valentine Affair linalotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa King Solomon jijini Darv Salaam katika siku ya Wapendanao Jumapili hii.
Akiongea na wanahabarti, Mratibu wa Matukio wa kampuni ya King Solomon Events, Bi Hellen Kazimoto amesema Kampuni hiyo inayokuja kwa kasi katika mambo ya burudani, baada ya kukonga nyoyo za mashabiki kwa matamasha yake yaliyoonesha mapinduzi katika sekta ya burudani nchini, yakiwemo ya Party in The Parking na ziara ya mwanamuziki WizKid jijini Dar es salaam, sasa wanakuja na tamasha jingine kubwa zuri na la kusisimua katika msimu huu wa wapendanao.
Tamasha limepewa jina la Valentine Affairs ambapo litawapa nafasi wapenda burudani na wapendanao kwa ujumla kujumuika pamoja kwa ajili ya chakula chenye hadhi ya nyota tano na muziki wa kutumia ala utakaoshirikisha wanamuziki mahiri wa miondoko laini nchini, wakati huo huo zawadi za aina yake zikitolewa ukumbini hapo.
Onesho hilo litakalofanyika katika ukumbi wa King Solomons, Jumapili ya Tarehe 14 Februari, 2016, kuanzia saa 12 jioni na kuendelea linatarajiwa kupambwa na wanamuziki BenPol, Grace Matata pamoja na mkongwe Patricia Hillary.
Wanamuziki hawa watakuwa wakipigiwa muziki maalum kwa ajili ya wapendanao kwa vyombo vya ala, na watakuwa wakiburudisha wapendanao muda wote watakapokuwa katika eneo la tukio kuanzia kuwasili kwao, mpaka muda wa chakula n ahata wakati wa kupeana zawadi.
Zawadi zitakazotolewa ni pamoja na pete kwa wapendanao watakaokuwa na bahati, ni Pete yenye thamani ya shilingi Milioni nne, iliyotengenezwa kwa madini ya tanzanite, kutoka Gift Jewelers. Zawadi nyingine ni malazi ya siku mbili kwa wapendanao katika Hoteli ya Regency Park Hotel ambao pia ni wadhamini wa onesho hilo la aina yake ya wapendanao.
Zawadi nyingine ni vocha yenye thamani ya shilingi laki mbili za kitanzania kutoka kampuni ya King Solomons ambayo inaweza kutumika katika mgahawa wa Eaters Point au Wantashi.
Usiku huu wa Valentine Affair umefanikishwa na wadau mbali mbali kwa kushirikiana na King Solomons Events ambao ni Wantashi, Coca Cola, Eaters Point, EATV,EARadio,Regency Park Hotel,Gift Jewelers pamoja na twenty4 Printers.
PICHANI JUU: Kuroka kushoto Mratibu wa matukio wa King Solomon Events, Bi Hellen Kazimoto, Ben Pol, Patricia Hillary na muwakilishi wa Mgahawa wa eaters Point Chef Suba