Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), limesema litaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuhakikisha kwamba taifa linakuwa na wananchi wenye uwezo mkubwa wa kuvumbua na kutumia elimu.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa wa Unesco nchini Al Amin Yusuph wakati akizungumza na washiriki wa kongamano maalumu wa kupitia waraka wa mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu.
Kongamano hilo ni moja ya mradi wa CFIT wa UNESCO na serikali ya China wenye lengo la kusaidia serikali ya Tanzania kuimarisha umahiri wa wakufunzi na walimu kwa kuwawezesha kujua Tehama na kuitumia.
Mradi huo umelenga kuongeza uwezo wa vyuo vya walimu na teknolojia ya kisasa ya Tehama na vifaa vyake ili kusaidia kujifunza na kufunza.
Ingawa kwa sasa vyuo vinavyofanyiwa kazi na mradi huo vipo viwili vya Tabora na Monduli vipo vingine vinane vinavyofunza walimu wa sayansi na hesabu ambavyo vitaingizwa.
Yusuph aliwataka wadau wanaoshiriki katika kongamano ambalo lilitarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki kutekeleza wajibu wao kwa makini kwa kuwa Watanzania wanasubiri maelekezo yao kufanikisha utoaji wa elimu ya Tehama yenye kuleta mwelekeo mpya wa matumizi kwa kulenga kuvumbua na kutumia elimu kwa manufaa ya taifa.
Alisema UNESCO ipo tayari kuhakikisha kwamba Tanzania inazalisha wanafunzi ambao watakuwa na uwezo mkubwa katika Tehama ambao utaibua maendeleo endelevu.
“Si kutoa walimu wazuri tu bali kuwezesha jamii, wanafunzi na waliopitia mafunzo hayo kuwa na namna mpya ya kufikiri na kuvumbua vitu vipya vya kujiendelea na kuendeleza taifa” alisema Yusuph.
Alisema kimsingi elimu inatoa asilimia 5 lakini maisha yanatoa asilimia zilizobaki kama mtu atatumia vyema msingi wa maarifa aliyopewa.
Alifafanua kwamba Mradi huo ambao awali ulifadhiliwa na Benki ya Dunia na kukamilika mwaka 2011, haukuridhiwa kutumika hadi mwaka jana ulipokuja mradi wa CFIT ambao uliingizia upitiaji upya wa mradi huo na kuwezesha kuridhiwa kwa matumizi.
Naye kiongozi wa timu iliyopitia awali katika mradi huo wa CFIT, Profesa Ralph Masenge amesema wataalamu waliohusika na upitiaji huo kabla ya kongamano walitoka Chuo cha Ualimu Tabora na kile cha Monduli,Chuo kikuu huria Tanzania na Chuo kikuu cha Dar es salaam.
Alisema awali walipitia kuona mahitaji maalumu ya walimu kisha wakaja na mapendekezo ambayo sasa yanafanyiwa kazi. Alisema matatizo mengi ya elimu Tanzania yanatokana na uhaba wa vifaa vya elimu na ubora wa walimu.
Alisema mradi huo utasaidia kutoa elimu bora kwa kuwa na walimu bora na vifaa bora kupitia Tehama. Alisema mradi huo utasaidia kuwezesha Tehama kutumiwa kama chombo cha kutumia wanafunzi hasa pale panapokosekana.
Profesa Masenge alisema hatua waliyofikia ni hatua ya matayarisho na kwamba ni matarajio yao kwamba wakishafikisha hati hiyo kwa wizara masuala ya matumizi ya maabara yatakuwa yamekamilika.
Alisema lengo la mradi huo ni kuwezesha wanafunzi na walimu wao kuongeza maradufu uwezo wao katika elimu.
Naye Mratibu wa kitaifa wa Mradi Wa CFIT Kutoka UNESCO, Faith Shayo alisema kongamano hilo ni sehemu ya maandalizi ya mafunzo na matumizi ya maabara katika vyuo vya Monduli na Tabora katika kufunza Tehama ili kuboresha mafunzo na ufundishaji.
“Leo tuko hapa Bagamoyo kwa ajili ya wadau kudiscuss ICT draft document (kujadili hati hii yenye draft ya mafunzo) ambayo ilipitiwa na watu watano kabla ya kuikabidhi kwa Wizara ya Elimu “ alisema Faith.
PICHANI JUU: Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph, akielezea mantiki ya warsha ya wadau wa elimu kuhusu viwango vya umahiri wa Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu Tanzania iliyofanyika mjini Bagamoyo, mkoa wa Pwani mwishoni mwa juma.
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa CFIT kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Faith Shayo akifafanua jambo kwa wadau wa kongamano la kupitia kitabu cha mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu nchini lililofanyika mjini Bagamoyo, Pwani mwishoni mwa juma.
Jaco Du Toit, kutoka ofisi za Unesco kanda ya Nairobi akiendesha majadiliano ya maboresho ya vipengele mbalimbali vya waraka wa mafunzo ya Tehama kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu"UNESCO ICT Competency Framework for Teachers in Tanzania" wakati wa kongamano hilo lililomalizika mwishoni mwa juma mjini Bagamoyo.
Pichani juu na chini ni washiriki wakiwasilisha mawazo yao wakati kongamano likiendelea kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha waraka huo.
Washiriki wa kongamano hilo wakifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiwasilishwa.