Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Waziri W.Kindamba akikabdhi msaada wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Tandale kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Tandale Dkt Emmanuel Kazimoto na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Mheshimiwa Ally Hapi.
Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Mheshimiwa Ally Hapi akizungumza kwenye hafla ya kupokea msaada wa dawa na vifaa tiba kutoka Kampuni ya Simu Tanzania(TTCL). Katika Haflya hiyo ilihudhuriwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Bw Waziri W.Kindamba, Dr Zuhura Majapa Mratibu wa BRN Manispaa ya Kinondoni na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Tandale Dkt Emmanuel Kazimoto.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Waziri W.Kindamba akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa dawa na vifaa tiba kwa Kituo ch Afya cha Tandale, wilayani Ilala, jijini Dar es salama
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto katika sekta mbali mbali nchini ili kuboresha huduma za Kijamii zinazogusa maisha ya kila siku ya Wananchi kwa lengo la kuyaboresha na kuongeza kasi ya Nchi kupiga hatua za Maendeleo.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar Es Salaam na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw Waziri Kindamba alipokuwa akikabidhi msaada wa dawa na vifaa tiba kwa Kituo cha Afya cha Tandale, kilichopo Wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es salaam mwishoni mwa wiki hii.
Msaada huo umekabidhiwa kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Tandale Dkt Emmanuel Kazimoto, tukio lililoshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya Kinondoni Mheshimiwa Ally Hapi ambaye ndie aliwezesha kupatikana kwa vifaa hivyo kupitia program yake maalumu ya kuwasiliana na Taasisi za Umma na Binafsi ili zisaidie kuboresha huduma za kijamii Wilayani kwake.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Kituo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi ameishukuru Kampuni ya Simu TTCL kwa msaada iliotoa na kubainisha kuwa, msaada wa dawa na vifaa tiba utasaidia sana kuboresha huduma katika kituo hicho chenye kuhudumia idadi kubwa ya Wananchi wa kipato chini.
“Juhudi hizi za kusogeza huduma kwa wananchi ni muhimu sana katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuboresha maisha ya watu wa hali ya chini na kuwaondoa katika unyonge unaowafanya kushindwa kutoa mchango stahiki katika jitihada za nchi kujiletea Maendeleo” Amesema Mhe Hapi
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameutaka uongozi wa Kituo cha Afya Tandale kuhakikisha kuwa unasimamia vyema matumizi ya dawa hizo ili zitumike kwenye malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kuboresha huduma kwa Wananchi.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Bw. Waziri W.Kindamba amesema, TTCL imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia Jamii kwenye sekta mbalimbali kama vile elimu, afya, michezo, matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano, makundi maalum na wakati wa maafa.
“TTCL imetoa msaada huu wenye thamani ya shilingi milioni 5, dawa zilizotolewa ni pamoja na Paracetamol Syrup, Paracetamol Tabs, Diclofenac, Amoxicillin, Amoxicillin Granules, Folic Acid, Gloves Surgical, Bandage, Magnesium Trisilicate, Methylated Spirit na nyinginezo nyingi. Tunaamini kuwa msaada huu utatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba wa dawa kwenye kituo hiki” amesema Waziri K.Kindamba.
Aidha, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Bw. Waziri W.Kindamba ametoa rai kwa taasisi na makampuni mengine kukusaidia juhudi za Serikali katika kusaidia huduma za Kijamii hali itayoimarisha uhusiamo mwema na Wananchi na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili jamii katika maeneo mbali mbali nchini.