Bunge la Israel limepitisha sheria ya kuhalalisha maeneo ya makazi ya Wayahudi yaliyoko Ukingo wa Magharibi, licha ya kulaaniwa na jumuiya ya kimataifa kwa kukiuka katiba.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, nyumba 3,850 zilizojengwa bila idhini kwenye ardhi ya Palestina zitahalalishwa.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema atapiga kura ya ndio baada ya kurudi Israel kutoka kwenye mkutano na mwenzake wa Uingereza Bibi Theresa May.
Kabla ya upigaji kura, mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov ameonya kwamba sheria hiyo itakuwa na athari kubwa kwa Israel, na pia inaweza kuathiri mchakato wa amani kati ya waarabu na waisrael.
Mashirika mawili ya haki za binadamu ya Israel Peace Now na Yesh Din yamesema yatawasilisha mahakamani ombi la kufuta sheria hiyo.