Wakazi wa vijiji vya Hembeti na Dihombo wakisubiria kupata Hati miliki zao.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi akitoa hotuba yake wakati wa alipozindua utoaji wa Hatimiliki za kimila wilayani Mvomero.
Mratibu wa Elimu kata ya Hembeti, Charles Kikully akisoma Risala ya vijiji vya Hembeti na Dihombo kwa Waziri Lukuvi.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mh. Mohamed Utali akizungumza jambo wakati wa uzinduzi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Bw. Rugembe Maige akitoa taarifa ya wataalam ya Wilaya ya Mvomero na Tume ya Matumizi na Mipango ya Ardhi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Dkt. Stephen Kebwe Akiongea na wananchi wakati wa uzinduzi wa utoaji hati za Kimila.
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Mipango na Matumizi ya Ardhi Dkt. Stephen Nindi akiwatambulisha wageni walioongozana na Mh. waziri Lukuvi kwa wanakijiji wa Hembeti na Dihombo.
Mwenyekiti wa Tume ya Mipango na matumizi ya Ardhi Bw. Fidelis Mutakyamilwa akitoa neno la shukurani kwa Waziri Lukuvi kwa kuzindua rasmi utoaji wa Hakimiliki za Kimila, pia kutoa shukurani kwa viongozi mbalimbali, wadau na wananchi waliojumuika katika uzinduzi huo.
Wananchi mbalimbali wa Kijiji cha Hembeti na Dihombo wakikabidhiwa Hati za Kimila na Mh. Waziri Lukuvi.
Baadhi ya wanakijiji wakisoma Hati zao.
Wanakazi wa Mvomero pamoja na wadau mbalimbali wakiwa katika uzinduzi huo.
Baadhi ya wanavijiji vya Hembeti na Dihombo wakiwa katika picha ya pamoja na Mh. Waziri Lukuvi mara Baada ya kumaliza zoezi la Ugawaji wa Hati hizo.
Picha na Fredy Njeje.
Na Hembeti Wilayani Mvomero, Morogoro.
Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi,(MB) amezindua rasmi utoaji wa Hati Miliki za ardhi za Kimila katika vijiji viwili vya Hembeti na Dihambo wilayani Mvomero mkoani Morogoro ambapo amegawa hati 1361 baada ya kupima vipande vya ardhi 2944.
Akizungumza na wanakijiji hao Waziri Lukuvi alisema kuwa ameamua kuja mwenyewe kuzindua ugawaji wa hati miliki ili apate kujiridhisha na kuona kazi hiyo imefanyika kitimilifu na kutekelezwa kama alivyo agiza, alisema kazi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kuhakikisha nchi inapangwa kwa kupima ardhi yake ambapo wananchi watapimiwa ardhi na kupewa hati za kumiliki maeneo hayo, na kusisitiza kuwa baada ya kukabidhiwa Ardhi hiyo ulinzi wa ardhi hiyo utakuwa ni juu ya mmiliki mwenyewe.
Alisema kuwa njia moja wapo ya kuondoa migogoro ya ardhi ni kuhakikisha kuwa kila Mwanakijiji anamiliki kipande chake cha ardhi kwa kuwapatia hati za kimila na kwamba pamoja na kugawa hati hizo bado wataalam watabaki kuendelea kupima ardhi mpaka watakapo kamilisha zoezi hilo la kupima na kutoa hati za vipande 5200 ambapo vijiji vitakavyoendelea kupimwa ni pamoja na Hembeti, Ihombo,Bungoma,Kindo na Kibugu pia kijiji cha Kambala ambacho nacho kipo tayari kwa ajili ya kuanza kupimwa ambapo watapanga matumizi bora ya Ardhi na kutoa hati, ambapo matumizi hayo ya ardhi yataainisha maeneo ya Kilimo na Ufugaji.
Na kwa maeneo ya kilimo wafugaji hawataruhusiwa kulishia mifugo yao. Waziri Lukuvi amesisitiza katika eneo la kambala watakapopima eneo la mifugo ni lazima wataalam waainishe na idadi ya Mifugo watakao fugwa katika eneo hilo pamoja na kuweka miundombinu kama josho la Kuogeshea na mabwawa ya kunyweshea maji ambapo wananchi nao watapaswa kuchangia gharama kidogo ili kuepuka muingiliano baina yao na wakulima.
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa Wilaya ya Mvomero ndio Wilaya pekee nchini Tanzania ambayo Serikali imefanya matumizi bora ya Ardhi kwa vijiji vingi zaidi kulipo wilaya yoyote Tanzania na mpaka sasa yamefanyika matumizi bora ya ardhi katika vijiji 73 Mvomero,na kusisitiza kuwa ardhi ya Mvomero bado ina rutuba hivyo hawana sababu ya kungojea ruzuku ya mbolea kutoka serikalini. Pia Waziri amewaonya madiwani wasigawe tena vijiji pindi uchaguzi unapokaribia kwa kufanya hivyo watakuwa wameharibu utaratibu wa vijiji ambavyo tayari vimepimwa kwa kuwa ugawaji huo hauwasaidii wananchi katika maendeleo bali huwanufaisha wanasiasa wanaotaka vyeo.
Sambamba na hilo amewasihi waliopata hati hizo kuwa thamani yake ni kubwa zaidi kulipo ardhi ambayo haijapimwa kwa kuwa kupitia ardhi hiyo mwanakijiji anaweza kutumia hati hiyo kwa ajili ya kupata mkopo Benki, amewataka wale wanaokaidi kushiriki katika zoezi za upimaji na matumizi ya ardhi na wao washiriki kwa sababu mpango wa matumizi ya ardhi una faidia kubwa.
"Mpango huu wa upimaji unaendelea wilaya za Kilombelo, Ulanga na Malindi ambapo watapanga kupima na kutoa hati laki tatu (300,000) na kumalizia kuwa kila mtu ambaye amepewa hati yake haruhusiwi kuiuza kwa mtu yoyote nje ya mwanafamilia wa kijiji ambapo ndipo kuna mmiliki wa ardhi hiyo na kuwasisitiza wale wote walio nje ya Mkoa wa Morogoro wafike pindi matumizi ya ardhi na upimaji wanapofika katika maeneo yao." alisema Waziri Lukuvi.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Dkt. Stephen Kebwe akiongea na wanakijiji hao alisema kuwa mtu yeyote atakae jaribu kuleta migogoro ya ardhi Serikali haita wafumbia macho na Sheria itachukua mkondo wake kwa kuwa hao ndio wanaorudisha nyuma maendeleo.