Beki wa pembeni na nahodha wa klabu bingwa nchini Ujerumani FC Bayern Munich Philipp Lahm amethibitisha atashaafu soka mwishoni mwa msimu huu.
Lahm alitoa uthibitisho huo mara baada ya mchezo wa kombe la la nchini Ujerumani dhidi ya Wolfsburg uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo, ambapo FC Bayern Munich walichomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri.
Mwishoni mwa juma lililopita, Lahm alicheza mchezo wake wa 500 tangu alipoanza kuitumikia klabu Bayern Munich, mwaka 1995 akiwa na kikosi cha vijana na baadae alipandishwa na kucheza kwenye kikosi cha wakubwa mwaka 2001.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 33, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, anaamini mwishoni mwa msimu huu utakua muda muafaka kwake kufanya maamuzi wa kustaafu.
"Nitastaafu soka mwishoni mwa msimu huu," Alisema Lahm. "Nimesha utaarifu uongozi kuhusu maamuzi haya.
"Nimefanya maamuzi haya kwa kuamini kuna nafasi nyingine ya kuendelea kuutumikia mchezo wa soka, kwa sasa ninafikiria kuingia kwenye uongozi ili niweze kutoa mchango kwa wenzagu watakaokuja baadae, Nitahakikisha katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu ninafanya kila linalowezekana ili tufanikiwe kutwaa ubingwa wa michuano yote tunayoshiriki," Aliongeza Lahm.
Lahm alitangazwa kuwa nahodha wa FC Bayern Munich mwaka 2011 baada ya kuondoka kwa Mark van Bommel, na baadae alipewa cheo hicho upande wa timu ya taifa, na alifanikiwa kuwaongoza wenzake kutwaa ubingwa wa kombe la dunia mwaka 2014.
Ametwaa ubingwa wa ligi ya nchini Ujerumani (Bundesliga) mara saba, Ubingwa wa kombe la Ujerumani (DFB-Pokals) mara sita, ligi ya mabingwa barani Ulaya (Champions League) mara moja, ubingwa wa klabu bingwa duniani (FIFA Club World Cup) mara moja na ubingwa wa kombe la dunia (FIFA World Cup)mara moja.