Mjomba wa mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Sadio Mane, ametoa taarifa za kuhofia usalama wa familia yake baada ya mpwa wake kukosa penati na kusababisha Senegal kutolewa kwenye michuano ya AFCON iliyomalizika nchini Gabon mwanzoni mwa mwezi huu.
Mane alikosa penati katika mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya Cameroon, ambao walichomoza na ushindi wa Penati Tano kwa nne, baada ya kwenda sare ya bila kufungana katika dakika 120.
Sana Toure amesema gari alilonunuliwa na mpwa wake Mane, ambaye ndiye mchezaji ghali zaidi barani Afrika, liliharibiwa na nyumba yake kulengwa.
"Siku baada la Lions kuondolewa, baadhi ya watu walio na nia mbaya wakataka kuvamia nyumba yangu iliyo Malika. Nawashukuru majirani na wenyeji, kitu kibaya kilizuiwa." Sana Toure alivyambia vyombo vya habari.
Sadio Mane alionekana kusahau yaliyomsibu wakati wa fainali za AFCON na kufunga mabao mawili wakati wa mchezo wa Liverpool dhidi ya Tottenham Hotspurs mwishoni mwa juma lililopita.