
Mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa kundi la G20 ulifunguliwa jana mjini Bonn, Ujerumani, ikiwa ni hatua ya maandalizi ya mkutano wa kilele wa kundi hilo utakaofanyika mwezi wa Julai mjini Hamburg.
Kwenye mkutano huo washiriki wamezungumzia masuala ya kutimiza ajenda ya maendeleo endelevu, kulinda amani na kuimarisha ushirikiano na Afrika.
Msemaji wa mambo ya nje ya China Bw. Geng Shuang amesema China inapenda kushirikiana na nchi nyingine kufanikisha mkutano huo na kukabiliana kwa pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia.
Naibu chansela wa Ujerumani na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Sigmar Gabriel amesema kwenye mkutano huo nchi mbalimbali zinatakiwa kushirikiana kuchunguza vyanzo vya migogoro na kutafuta njia ya amani ya kuzuia na kutatua masuala hayo.
Mbali na nchi wanachama, nchi na mashirika mengine kama Singapore, Umoja wa Mataifa, APEC na AU wamealikwa kushiriki kwenye mkutano huo.