
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri Hector Cuper amesema hana muda wa kupoteza kwa sasa, zaidi ya kufikiria namna ya kuiwezesha timu yake kufuzu fainali za Afrika za 2019 na zile za kombe la dunia za 2018.
Cuper ambaye alikishuhudia kikosi chake kikishindwa kutwaa ubingwa wa Afrika mwanzoni mwa mwezi huu, kwa kufungwa na Cameroon mabao mawili kwa moja, amesema wakati uliopo ni sahihi kwake kuhakikisha wachezaji wanakua tayari kwa mapambano.
Amesema wakati mwingine baadhi ya mashabiki wa soka nchini Misri hudhani maandalizi ya timu ya taifa huchukua nafasi juma moja ama mawili kabla ya mchezo husika, lakini jambo hilo kwake halipo kutokana na dhamira aliyojiwekea ya kuhakikisha anafuzu kucheza fainali zote mbili.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Argentina ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau wa michezo nchini Misri, ili kufanikisha azma ya maandalizi ya kikosi chake.
Katika harakati za kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018, Misri imepangwa kundi E na timu za Uganda, Congo Brazzaville na Ghana.
Misri inongoza kundi hilo kwa kufikisha pointi sita zilizotokana na ushindi dhidi ya Congo Brazzaville na Ghana.
Kwa upande wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2019, Misri wamepangwa kundi J na Tunisia, Niger na Swaziland.