Klabu ya Rotary ya Oyster Bay imeandaa kambi ya matibabu ya bure itakayofanyika eneo la Kerege wilayani Bagamoyo. Huduma hizo za matibabu zitatolewa siku ya Jumapili tarehe 27 Novemba katika shule ya Msingi ya Kerege.
Timu ya wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali, wanafunzi wa udaktari, wanachama wa Rotary na wafanyakazi wa kujitolea kutoka sekta mbalimbali watashiriki katika kambi hiyo ya matibabu.
Vipimo na matibabu yatatolewa kwa magonjwa kama malaria, upungufu wa damu, kisukari na shinikizo la damu, masikio, pua na koo (ENT), magonjwa ya ngozi, macho, meno na kansa ya kizazi kwa akina mama. Miwani zitatolewa kwa watu watakaokutwa na matatizo ya macho. Huduma za ushauri kwa wajawazito zitatolewa na wajawazito pia watapatiwa vifaa vya kujifungulia bure.
Wakazi wa Kerege na maeneo ya jirani wanaombwa kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo ya matibabu ya bure haswa akina mama na watoto.
Akizungumza kuhusu mradi huu, Alfred Woiso, Rais wa Klabu ya Rotary ya Oyster Bay alisema, “Tuna furaha kuandaa kambi hii kwa mara nyingine tena kwa wakazi wa Kerege ambapo lengo letu ni kuwasaidia watu ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu. Tunawashukuru wadhamini na watu wote wanaojitolea katika mradi huu na tunakaribisha watu kuhudhuria na kusaidia kwa namna yoyote ile katika kambi hii ya matibabu.”
Usajili wa matibabu utaanza mapema asubuhi na watu wapatao 1,200 wanatarajiwa kupata huduma za matibabu kulingana na mwenendo wa idadi ya watu ambao huwa wanajitokeza kila mwaka kambi hiyo inapofanyika. Wakazi wa Kerege wanashauriwa kufika mapema ili kuweza kupata huduma.
Kambi hiyo ya matibabu imedhaminiwa na Diamond Trust Bank na inaandaliwa kwa ushirikiano na Shree Hindu Mandal Hospital, Vital Supplies, Whitedent, vClick Concepts Inc, MAK Books and Brains, ABACUS Pharmaceuticals, Fazel Foundation na wanachama wa Klabu ya Rotary na Rotaractor.