Jackie Evancho, mshindi wa pili katika shindano la kutafuta watu wenye vipaji la America's Got Talent ndiye atakayeongoza wimbo wa taifa wakati wa kuapishwa kwa Donald Trump.
Msichana huyo wa miaka 16 amesema ana furaha sana kwa kuchaguliwa kuongoza wimbo huo wa taifa wakati wa sherehe hiyo tarehe 20 Januari.
Boris Epshteyn, mkurugenzi wa mawasiliano wa kamati inayofanya maandalizi ya sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Bw Trump, amesema msichana huyo atawapa moyo Wamarekani wote.
Mwitaliano Andrea Bocelli na rapa Kanye West, ni miongoni mwa wasanii wengine ambao inadaiwa huenda wakatumbuiza siku hiyo.
Kanye West alikutana na rais huyo mteule katika jumba la Trump Tower jijini New York Jumanne.
Hata hivyo, hakujatolewa thibitisho kuhusu iwapo wawili hao walijadiliana kuhusu sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Trump.