↧
Fikile Mbalula: Zuma Hamuungi Mkono Issa Hayatou
Waziri wa michezo wa Afrika Kusini Fikile Mbalula amekanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kumuunga mkono Rais wa shirikisho la soka barani Afrika (CAF) Issa Hayatou katika uchaguzi mkuu, ambao umepangwa kufanyika mwezi ujao mjini Adis Ababa- Ethiopia.
CAF walisambaza taarifa katika vyombo vya habari mwishoni mwa juma lililopita, wakidai Rais Zima anakubaliana na utendaji kazi wa Hayatou na anamuunga mkono katika harakati zake za kutetea nafasi yake.
Taarifa hizo ziliibuliwa kufuatia kikao kilichowakutanisha rais Zuma na Hayatou Afrika Kusini kabla ya mchezo wa kuwania African Super Cup uliochezwa mjini Pretoria kati ya Mamelodi Sundowns (Afrika kusini) dhidi ya TP Mazembe (Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).
Taarifa iliyotolewa na waziri wa michezo wa Afrika kusini imeeleza kuwa: “Rais Zuma hakuzungumza lolote kuhusu kumuunga mkono Hayatou kwenye uchaguzi mkuu wa CAF, na ameshangazwa kuona taarifa hizo zikisambazwa kwenye vyombo vya habari.”
“Rais Zuma alimtakia kheri na fanaka Hayatou pamoja na wagombea wengine katika uchaguzi huo na wala hakumaanisha salamu hizo ni kwa mtu mmoja pekee.”
“Rais Zuma ni mwanamichezo na yupo tayari kushirikiana na yoyote atakaechaguliwa kwa ajili ya kuliongoza shirikisho la soka barani Afrika CAF.”
Hayatou ambaye ni raia wa Cameroon alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuliongoza shirikisho la soka barani Afrika mwaka 1988, na amekua madarakani mwa miaka 29.
Hayatou mwenye umri wa miaka 70, aliwahi kupata upinzani katika chaguzi mbili za CAF dhidi ya Armando Machado kutoka nchini Angola na Ismael Bhamjee wa Botswana na aliwashinda kwa kupata kura nyingi.
Katika uchaguzi mkuu wa CAF wa mwaka huu, Hayatou anatarajia kupata upinzani kutoka kwa Ahmad Ahmad wa Madagascar, ambaye amepewa baraka na nchi wanachama wa baraza la vyama vya soka kusini mwa Afrika COSAFA.
↧