Wataalamu wamshauri Clinton kutaka kura zihesabiwe upya
Kundi la wataalamu wa masuala ya uchaguzi na waliobobea katika masuala ya kompyuta, wamemwendea aliyekuwa mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais uliopita nchini Marekani Bi Hillary Clinton, kumfahamisha juu ya uwezekano wa kuchezewa kwa matokeo katika majimbo matatu muhimu. Wataalamu hao ambao ni pamoja na wakili wa haki ya kupiga kura John Bonifaz na gwiji wa masuala ya kompyuta J. Alex Halderman, wamesema wameng'amua dalili zinazozua mashaka katika mfumo wa mashine za kieletkroniki za kupigia kura katika majimbo hayo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na jarida la New York Magazine Jumanne.
Ingawa wataalamu hao hawakupata ushahidi wa kutosha juu ya kufanyika uchakachuaji, wametoa hoja kuwa zipo sababu za kutosha za kuyatazama upya matokeo hayo, hususan kutokana na udukuzi uliofanywa katika kompyuta za Kamati Kuu ya Chama cha Democratic wakati wa kampeni, ambao serikali ya Marekani iliishutumu Urusi kuufanya. Kura zilizohesabiwa hadi sasa zinaonyesha Bi Clinton akimzidi Trump kwa zaidi ya kura milioni mbili.
Trump alishinda majimbo ya kushindaniwa, na kupata kura nyingi za wajumbe.
Mfumo wa kura za wajumbe humfaa zaidi mgombea ambaye anashinda, hata kama kwa kura chache, katika majimbo mengine dhidi ya yule anayeshinda kwa kura nyingi katika majimbo machache.